Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAZI WA LONDONI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MRADI WA MAJI


Mhandisi Vicent Bahemana kulia akiwa na baadhi ya viongozi wa kata ya lizabon wakati wa kukabidhi mabomba ya mradi wa maji katika mtaa wa Londoni
Baadhi ya mabomba yalioshushwa mtaa wa Londoni wakati wa utekelezaji wa mradi wa maji katika kata ya Lizabon Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Wananchi waliojitokeza kupokea mabomba ya maji mtaa wa Londoni maji ya Songea Mkoani Ruvuma
Gari lililobeba mabomba ya maji likiwasili katika mtaa wa Londoni kata ya lizabon Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Mhandisi. Vincent Bahemana akizungumza na wananchi wa mtaa wa Londoni wakati wa kukabidhi mabomba ya maji


Na Regina Ndumbaro - Ruvuma. 

Wakazi wa mtaa wa Londoni katika Manispaa ya Songea wameonyesha furaha yao kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi na salama unaofadhiliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Songea (SOUWASA). 

Mradi huo unalenga adha ya upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa maeneo ya Londoni na Sinai, na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5.

Akizungumza na wananchi wakati wa mapokezi ya mabomba ya maji, Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi. Vincent Bahemana, amesema mabomba hayo yameletwa kwa ajili ya kuanza kazi ya uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya maji kwa urefu wa kilomita 64.9. 

Kati ya hizo, kilomita 20 zitatumika katika eneo la Londoni na kilomita 44.9 kwa ajili ya eneo la Sinai. 

Bahemana ameeleza kuwa mradi huo pia unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa mita za ujazo laki mbili, uchimbaji wa visima, ujenzi wa banda la pampu mbili na mfumo wa kuchuja na kutibu maji katika eneo la Sinai.

Diwani wa Kata ya Lizaboni, Mhe. John Mbunda, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi wake kuhusu tatizo la maji. 

Ameeleza kuwa zaidi ya wakazi 400 watanufaika na huduma hiyo, huku akiwasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa mafundi na kutunza miundombinu ya mradi huo ili uweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.

Wananchi waliopokea mabomba hayo kwa shangwe na furaha wameeleza hisia zao kwa kumpongeza Rais Samia. 

Halima Kasimu na Asha Kombo wamemshukuru Rais Samia kwa "kuwatua ndoo kichwani" baada ya miaka mingi ya kuteseka kutafuta maji safi. 

Wamesema kuwa awali walikuwa wakilazimika kutumia maji yasiyo salama, jambo lililokuwa tishio kwa afya zao.

Aidha, wananchi hao wametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Damas Ndumbaro, na Diwani wao Mhe. Mbunda kwa kushirikiana na mamlaka husika kufanikisha mradi huo. 

Viongozi hao wamehimiza ushirikiano zaidi kati ya wananchi na mamlaka ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com