Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAJI MWAKAHESYA : WAANDISHI WA HABARI ZINGATIENI MAADILI NA SHERIA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Jaji Ntuli Mwakahesya akizungumza kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali katika Mkutano Mkuu wa SPC
Jaji Ntuli Mwakahesya akizungumza kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali katika Mkutano Mkuu wa SPC

Na Neema Paul – Shinyanga

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili na sheria wanaporipoti habari, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2025.

Akizungumza Aprili 5, 2025 katika mkutano mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Shinyanga uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa, Jaji Ntuli Mwakahesya kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali katika Mkutano Mkuu wa SPC amesema waandishi wanapaswa kuwa makini na uhakika wa vyanzo vya habari wanavyotumia ili kuisaidia jamii kupata taarifa sahihi zisizo na upendeleo.

“Mahakama iko tayari kutoa mafunzo kwa waandishi ili kuwajengea uelewa kuhusu sheria za uchaguzi na umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma yao. Jamii kupata habari sahihi ni haki ya kikatiba,” amesema Jaji Mwakihesa.

Katika mkutano huo, Afisa Habari kutoka makao makuu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Christopher Kibanka, amewapongeza waandishi kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu miradi ya TASAF, hususan kwa kaya masikini.

Amesema kuwa kupitia mpango huo, kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa kiwango cha umaskini kwa asilimia 8 miongoni mwa walengwa, huku wanawake wakionekana kujiamini zaidi na kushika nafasi za uongozi kupitia vikundi vya kuweka na kukopa vilivyoundwa kwa msaada wa TASAF.

Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga imefanya mkutano wake mkuu ambapo imejadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya klabu pamoja na kuwapitisha wanachama wapya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com