Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUVUMA YASAFIRISHA MAHINDI NA MAKAA YA MAWE, SERIKALI YACHUKUA HATUA KUDHIBITI AJALI


Makaa ya mawe mojawapo ya bidhaa inayosafirishwa Mkoani Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Songea Wlilman Kapenjama Ndile akizungumza na wananchi na madereva Wilayani Songea Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro -Ruvuma.

Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuwa kitovu cha usafirishaji wa mazao ya kilimo na madini, ambapo zaidi ya tani 70,000 za mahindi zinasafirishwa kwenda nchini Zambia, huku tani 10,000 zikielekezwa nchini Malawi.

Sambamba na hilo, zaidi ya malori 1,000 hubeba makaa ya mawe kwa siku moja kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, jambo linaloonyesha ukuaji wa haraka wa shughuli za uchumi katika sekta hizo.

Hata hivyo, ongezeko la malori barabarani limepelekea changamoto mbalimbali za usalama barabarani, hasa kwa watumiaji wa vyombo vidogo vya usafiri kama bodaboda na bajaji.

Msongamano mkubwa wa magari umekuwa chanzo kikuu cha ajali, hali inayohatarisha maisha ya wananchi wa kawaida wanaotegemea usafiri huo wa kila siku.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya mkoa wa Ruvuma imechukua hatua madhubuti kwa kugawa viakisi mwanga 300 kwa madereva wa bodaboda na bajaji.

Hatua hii imelenga kuboresha usalama barabarani kwa kuhakikisha vyombo hivyo vidogo vinaonekana kirahisi wakati wa usiku au katika mazingira ya mwanga hafifu, hivyo kupunguza hatari ya kugongwa na magari makubwa.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji viakisi mwanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman Kapenjama Ndile amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kila mtumiaji wa barabara anakuwa salama.

Ameongeza kuwa hatua za upanuzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya mkoa zinaendelea ili kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi katika shughuli za usafirishaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com