Mwenyekiti wa MISA-Tanzania Edwin Soko akizungumza - Picha na Kadama Malunde
Na Marco Maduhu,ARUSHA
WAANDISHI wa habari wamepewa mafunzo ya usalama na ulinzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yametolewa leo Aprili 28,2025 katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yanayoendelea jijini Arusha.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-Tanzania), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Jamii Africa na Chama cha Waandishi wa Habari za Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT).
Mwenyekiti wa MISA-Tanzania Edwin Soko, amesema mafunzo ya usalama na ulinzi kwa waandishi wa habari ni muhimu sana, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia usalama wao.
"Mafunzo ya usalama na ulinzi kwa waandishi wa habari, ni muhumu sana katika utekelezaji wa majukumu yao ili wapate kuwa salama,"amesema Soko.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo imeendelea kushughulikia madhira yanayowakumba waandishi wa habari kazini, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria, kuwadhamini na kuwawekea Mawakili katika kesi zinazowakabili.
Kwa upande wake Afisa Programu kutoka UTPC Victor Maleko, akiwasilisha ripoti ya hali ya usalama wa waandishi wa habari kwa mwaka 2024, alisema waandishi 26 waliripotiwa kukumbana na madhila kazini, wakiwemo wanaume 22 na wanawake 4.
Victor Maleko
Amebainisha kuwa mikoa ya Mwanza na Dodoma inaongoza kwa matukio hayo.
Naye, Emmanuel Mkojera kutoka Jamii Africa akiwasilisha mada kuhusu usalama wa waandishi, aliwasisitiza waandishi kuwa makini na vifaa vyao vya kazi, akieleza kuwa vifaa hivyo ikiwemo simu na kompyuta ni sehemu muhimu ya ulinzi wao.
Emmanuel Mkojera
Mwenyekiti Mstaafu wa MISA-Tanzania na Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, ameipongeza MISA-Tanzania, UTPC, Jamii Africa na OJADACT kwa mshikamano wao katika kusaidia waandishi wa habari wanaopitia changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Salome Kitomari
Mkurugenzi wa UTPC Kenneth Simbaya, amesoma maazimio yaliyopendekeza wakati wa mjadala kwamba kuwepo kwa ushirikiano mkubwa zaidi kati ya Serikali na wadau wa habari kuhusu masuala ya ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi za habari.
Kenneth Simbaya
Maadhimisho haya ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yataendelea kesho kwa siku ya pili yakibeba kaulimbiu isemayo:
"Athari za Akili Bandia kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Tasnia ya Habari."
Soma pia :
Social Plugin