@malundeblog Watch on TikTokMvua yaleta madhara Kahama, yasababisha kifo https://www.malunde.com/2025/04/Mvua-Majanga.html
♬ original sound - Malunde
Na Mwandishi wa Malunde 1 blog – Kahama
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga zimeleta maafa makubwa, ikiwemo kifo cha binti mwenye umri wa makadirio ya miaka 16-19, ambaye bado hajafahamika jina wala makazi. Binti huyo amefariki dunia baada ya kusombwa na maji kwenye mtaro uliokuwa umejaa maji wakati akijaribu kuvuka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Aprili 6,2025 na kusema kuwa binti huyo alisombwa na maji ya mvua baada ya kuzama kwenye mtaro wa uliokuwa umejaa maji wakati akijaribu kuvuka.
“Niwaombe wananchi kuwa waangalifu wakati wa kuvuka, hususani kwenye mitaro iliyojaa maji, kwani mvua hizi zinazonyesha kwa sasa zinakuwa na madhara. Hivyo ni budi wakawa waangalifu ili kuzuia ajali zisizo na tija,” amesema Kamanda Magomi.
Sambamba na hilo, Kamanda Magomi amesema mvua hiyo imeleta madhara mbalimbali ikiwemo maji kuingia katika Benki ya CRDB Tawi la Social Kahama, maduka mbalimbali ya wafanyabiashara pamoja na nyumba za wananchi baada ya mitaro kujaa maji.
Bernard Mahongo, Diwani wa Kata ya Majengo, amewataka wananchi kutotupa taka kwenye mitaro – hali ambayo inachangia maji kujaa na kusambaa katika makazi yao na kusababisha hasara, ikiwemo kuharibika kwa vyakula na thamani za ndani.
“Maeneo yalikumbwa na mafuriko. Wananchi wametupa taka kwenye mitaro. Serikali inatumia gharama kuijenga lakini sisi hatuitunzi. Wengine wanajenga ukuta na kuziba mitaro, hali ambayo mvua ikinyesha inaweza kusababisha madhara kama vile mafuriko. Kata ya Majengo zaidi ya nyumba 100 zimeathiriwa na maji,” amesema Mahongo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, amemuagiza Meneja wa TARURA Kahama kuhakikisha anashirikiana na mkandarasi anayejenga barabara kupitia Mradi wa TACTICS kuzibua mitaro ili kuzuia mafuriko katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.
“Zuieni ujenzi holela wa makazi, hususani wanaojenga katika njia za maji ili kuepusha madhara zaidi. Tumekagua na tumebaini watu wamejenga na kuziba mikondo ya maji, hali ambayo inahatarisha usalama wao na wa wenzao,” amesema Mhita.
Social Plugin