
Na Lydia Lugakila - Bukoba
KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) yenye lengo la kutoa elimu mbalimbali za kisheria pamoja na utatuzi wa migogoro kwa Wananchi, hasa wanyonge pamoja na makundi mbali mbali wanaokabiliwa na migogoro ikiwemo ya ardhi na mirathi inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Mkoani Kagera huku Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro akitarajiwa kuizindua rasmi mnamo April 14,2025 katika uwanja wa Mashujaa maarufu Mayunga.
Kampeini hiyo inalenga kuleta faraja kwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao watafika katika viwanja hivyo kutatuliwa changamoto walizonazo kwa muda mrefu ambapo watakutana na jopo la wanasheria kutoka wizarani, wanasheria kutoka asasi za kiraia, pamoja na mawakili wa kiserikali.
Mkurugenzi wa Kampeni hiyo (MSLAC), Ester Msambazi akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kagera amesema kuwa mpaka sasa kampeini hiyo imeisha tekelezwa katika mikoa 23 na mkoa wa 24 ni Tanga ambapo kampeini inaendelea na sasa ni zamu ya Mkoa wa Kagera ambapo itadumu kwa siku 9.
Amesema kuwa kuwa kila wilaya watafikia kata 10 kwa siku na vijiji 30, tunatarajia kufikia wananchi kwa asilimia 75 wenye migogoro ya ardhi ,mirathi Mkoani Kagera huku huduma zote za kisheria zikitarajiwa kutolewa bure ikiwemo uandikishaji wa vitambulisho vya taifa NIDA isipokuwa mwananchi atachangia kidogo katika upande wa huduma za rita zinazohusiana na usajiri wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo.
Msambazi amewaomba wananchi wa Mkoani humo kujitokeza kwa wingi na kuwasisitiza waitumie vyema siku hiyo muhimu kwani baadhi ya changamoto zao zitaisha pale pale.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta, Samia Suluhu Hassan kwani kampeini hiyo inaenda kumuhakikishia mwananchi mnyonge haki na usawa katika kupata haki zake za msingi
Pia ametoa wito kwa Wananchi mkoani humo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili kueleza changamoto zao.
Aidha Rc Mwassa amesema kampeini hiyo ni kabambe hivyo Wananchi wahakikishe hawabaki nyuma kwani anatambua wanakagera wanazo changamoto nyingi hasa za migogoro ya ardhi na mirathi ambazo baadhi walijaribu kuzitatua lakini nyingine zilikuwa nje ya uwezo wao.
"Niwaombe Wananchi siku ya Jumatatu April 14 saa mbili asubuhi msikose pale uwanja wa Mayunga ili shida zenu zitatuliwe kwa muda mfupi" ,alisema RC Mwassa.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa ameziagiza halmashauri za mkoa huo baada ya kuzindua kampeini hiyo waendelee kuwa na kliniki za kusikiliza kero ambazo zitakuwa zinafanyika kila siku ya Jumanne na Alhamis ambapo Mkuu wa wilaya na wataalam wake watakuwa wanakaa kusikiliza kero mbali za Wananchi katika maeneo yao.
Social Plugin