Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Mheshimiwa Saimon Chacha akikabidhi mashine ya kuchapisha na kutoa kopi pamoja na laptop wakati wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 22 wa Chama cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD)
Na Regina Ndumbaro - Tunduru.
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Brigedia Aloyce Mwanjile, amewataka viongozi na vyama vya ushirika kutendea haki wakulima kwa kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati.
Ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa kawaida wa Chama Kikuu cha Ushirika cha TAMCU Ltd, uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Brigedia Mwanjile amewashukuru washirika wa TAMCU kwa ushirikiano wao na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua tena kuendelea kuongoza bodi hiyo.
Katika hotuba yake, Brigedia Mwanjile amesema alipoteuliwa kwa mara ya kwanza, uzalishaji wa korosho ulikuwa umeshuka hadi tani laki moja na kidogo, lakini ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia tani 520,000.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya CCM kutoa pembejeo bure kwa wakulima pamoja na kazi kwa bidii na weledi inayofanywa na wakulima.
Hata hivyo, amewahimiza wakulima kuongeza usimamizi wa mashamba yao, kuondoa mapori, kutumia pembejeo kwa wakati na kuongeza ukubwa wa mashamba.
Kwa upande wa mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Saimon Chacha aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili mustakabali wa maendeleo ya TAMCU.
Amebainisha kuwa vyama vya ushirika vimefanikiwa kusimamia ukusanyaji na mauzo ya mazao mbalimbali kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Ametaja kuwa mauzo ya ufuta yalifikia tani 8,774.621 zenye thamani ya Shilingi 29.4 bilioni, mbaazi tani 9,696.960 zenye thamani ya Shilingi 17.05 bilioni, na korosho tani 31,608.038 zenye thamani ya Shilingi 93 bilioni.
Licha ya mafanikio hayo, Mheshimiwa Chacha Ameeleza changamoto zinazowakabili wakulima ikiwemo ucheleweshaji wa malipo kutokana na kutokamilika kwa taarifa za kibenki za baadhi ya wakulima, ucheleweshwaji wa vifungashio, na kuwepo kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu.
Ameagiza benki, vyama vya ushirika na taasisi husika kuwahamasisha wakulima kutumia akaunti za mazao ipasavyo, bodi ya korosho na vyama vikuu kuhakikisha vifungashio vinapatikana kwa wakati, na kuajiri watendaji waaminifu na wenye weledi.
Katika hatua nyingine, mkutano huo pia umetambua na kupongeza vikundi vilivyofanya vizuri kwa kuwazawadia mashine za kuchapisha na laptop zenye thamani ya Shilingi milioni sita na nusu.
Zawadi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Saimon Chacha kama motisha ya kuendeleza jitihada za maendeleo na ufanisi katika sekta ya ushirika.
Social Plugin