Afisa Habari na Mawasiliano kutoka TASAF Christopher Kidanka akizungumza kwenye mkutano mkuu wa SPC
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka TASAF Christopher Kidanka akizungumza mkutano mkuu wa SPC
Na Kadama Malunde - Shinyanga
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini nchini Tanzania, ambapo hadi kufikia Machi 2024, zaidi ya kaya milioni 1.3 zimenufaika kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) uliofanyika leo Aprili 5, 2025 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Afisa Habari na Mawasiliano wa TASAF, Christopher Kidanka, amesema mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia ruzuku za elimu, afya, na miradi ya uzalishaji mali.
"Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi nchini kimepungua kutoka asilimia 39.0 hadi asilimia 36.0, huku umaskini wa mahitaji ya chakula ukishuka kutoka asilimia 9.2 hadi asilimia 8.0",amesema.
Kidanka amebainisha kuwa kupungua kwa viwango hivyo ni uthibitisho wa mafanikio ya moja kwa moja ya utekelezaji wa mpango wa TASAF.
"Katika Mkoa wa Shinyanga pekee, kaya 33,691 zimefaidika na mpango huo, ambapo baadhi ya wanufaika wametumia ruzuku hiyo kununua vifaa vya shule kwa watoto wao, chakula, pamoja na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba kwa kutumia mbao au mabati badala ya nyasi. Zaidi ya shilingi bilioni 23 zimetolewa kama ruzuku kwa wanufaika katika halmashauri tatu za mkoa huo",ameongeza.
Amesema mbali na ruzuku, TASAF pia imewawezesha wananchi kupata mikopo kupitia ushirikiano na taasisi za kifedha kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na taasisi ya FESLIB.
Ameeleza kuwa, hadi sasa, zaidi ya watu 15,524 wamenufaika na mikopo hiyo kwa ajili ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuinua hali zao za maisha.
TASAF ilianzishwa mwaka 2000 kwa lengo la kupambana na umaskini nchini kwa kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mpango huo umeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika kuinua maisha ya Watanzania wanaoishi katika mazingira magumu.
Soma zaidi
Social Plugin