Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile akizungumza baada ya uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Bombambili Manispaa ya Songea
Makamu Mwenyekiti wa TEF Bakari Machumu akiwashukuru Wahariri Tanzania baada ya kushinda nafasi hiyo bila kupingwa Mkoani Ruvuma
Ana Mwakyosa akizungumza baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Bombambili Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kwa niaba ya wajumbe waliochaguliwa
Na Regina Ndumbaro -Malunde 1 blog Songea
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limefanya uchaguzi wake mkuu mkoani Ruvuma, na kwa mara nyingine, Deodatus Balile amechaguliwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Uchaguzi huo umefanyika leo kwa amani, huku wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakishiriki mchakato huo.
Kwa mara nyingine, Balile amepewa dhamana ya kuongoza TEF ikiwa ni ishara ya imani kubwa ya wanachama wa TEF kwa uongozi wake, katika kulinda na kukuza maslahi ya wanahabari nchini.
MISA TAN YAPONGEZA NA KUAHIDI USHIRIKIANO WA KARIBU
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tan), Edwin Soko, amepongeza uchaguzi huo na kusema kuwa ni uthibitisho wa umoja na utulivu ndani ya TEF.
“MISA Tan tunampongeza Mwenyekiti Deodatus Balile na kamati yake ya utendaji kwa kuchaguliwa tena kuongoza TEF. Hii ni imani kubwa waliyopewa na wanachama wa TEF, na ni uthibitisho kuwa uongozi wao umetenda vyema,” amesema Soko.
Ameongeza kuwa MISA Tan itaendelea kufanya kazi kwa karibu na TEF katika kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira bora na salama.
Kwa kuchaguliwa tena, Balile ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kulinda maslahi ya wanahabari na kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari nchini.
Social Plugin