Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAENDELEO YA MIUNDOMBINU YA BARABARA WILAYA YA TUNDURU YAPIGA HATUA KUBWA



Ofisi ya TARURA Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Meneja TARURA Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,Silvanus Ngonyani 
Meneja TARURA Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,Silvanus Ngonyani 

Na Regina Ndumbaro Tunduru. 

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tunduru, Silvanus Ngonyani, ameeleza mafanikio makubwa katika sekta ya miundombinu ya barabara ndani ya wilaya hiyo. 

Akizungumza leo ofisini kwake, Ngonyani amesema kuwa barabara kadhaa zilizokuwa hazipitiki hapo awali sasa zinapitika kwa urahisi baada ya kufanyiwa ukarabati, licha ya kuwa baadhi bado hazijakamilika kwa kiwango cha juu. 

Ametolea mfano wa barabara ya kutoka Kijiji cha Chemchem hadi Misechela na ile ya Kangomba kuelekea Njenga, ambazo sasa zinaweza kupitika bila matatizo kama ilivyokuwa awali.

Ngonyani ameeleza kuwa hali ya miundombinu ya barabara katika mji wa Tunduru imekuwa na changamoto kutokana na jiografia ya eneo hilo lenye mwinuko na udongo wa mchangamchanga, hali inayochangia kuharibika kwa haraka kwa barabara hasa kipindi cha mvua. 

Hata hivyo, amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu hiyo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kilomita 8 hadi 10 za barabara za lami zilizokamilika.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kati ya barabara 206 zilizopo wilayani Tunduru, ni barabara sita tu ambazo bado hazijakamilika. 

Amesema changamoto kubwa katika mji wa Tunduru ni pamoja na ukosefu wa mitaro ya kupitisha maji, jambo linalochangia uharibifu wa barabara. 

Aidha, ameeleza kuwa gharama za ujenzi na ukarabati wa barabara ni kubwa, na hivyo miradi mingi hufanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Ngonyani ametaja barabara za vijijini zenye changamoto kubwa kuwa ni pamoja na barabara ya Mkoela-Ngapa, Nakapanya-Turiani yenye daraja linalohitaji matengenezo, Mbesa-Mbati-Marumba, Lukumbule-Kazamoyo, Ligunga-Kindamba, na Mchuruka-Cheleweni ambazo zote zina changamoto ya vivuko. 

Ameeleza kuwa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo tayari zimetengwa na zipo tayari kutumika.

 Ngonyani amesema kuwa miradi ya barabara katika maeneo mbalimbali kama Kalanje na Mchangani bado haijakamilika kikamilifu na itachukua muda kidogo kabla ya kumalizika. 

Hata hivyo, amesema kuwa kazi kubwa imefanyika hadi sasa na juhudi za serikali ya awamu ya sita zinaonekana dhahiri katika kuboresha miundombinu ya barabara mijini na vijijini ndani ya Wilaya ya Tunduru.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com