Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI HAMIS MWINJUMA : VYOMBO VYA HABARI VINAPASWA KUWA HURU KWA MUJIBU WA SHERIA


 Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog Songea 

Naibu Waziri wa Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwa huru kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, huku vikizingatia maadili, weledi na nidhamu ya taaluma.

Akizungumza katika Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika leo katika Ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, Mwinjuma amesema uhuru huo wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kuimarisha demokrasia na kuwajibisha mamlaka, lakini unapaswa kwenda sambamba na utii wa sheria na kanuni za taaluma ya habari.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema nafasi aliyopewa katika serikali ni dhamana kubwa, na ameahidi kuendelea kuitumikia kwa weledi na uzalendo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na vyombo vya habari kwa maendeleo ya taifa.

Amepongeza viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, akiwemo Mwenyekiti Deodatus Balile na Kaimu Mwenyekiti Bakari Machumu, kwa kuandaa mkutano wenye mjadala wa kina unaogusia changamoto, fursa na mustakabali wa sekta ya habari nchini.

Mwinjuma amesema kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wanahabari katika kuelimisha jamii, kulinda misingi ya demokrasia, na kuchochea maendeleo, na hivyo itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao katika mazingira bora.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ametumia fursa hiyo kumkaribisha rasmi mgeni wa heshima wa mkutano huo, Dkt. Emanuel Nchimbi, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea mwenza wa Urais kupitia chama hicho, akisema ujio wake ni ishara ya kuthamini mchango wa wanahabari katika maendeleo ya taifa.

Amewatakia mafanikio wajumbe wa mkutano huo katika uchaguzi wa viongozi wa TEF, huku akieleza kuwa serikali itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa sekta ya habari kwa maslahi ya taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com