Na Dotto Kwilasa
Jumla ya wakulima wa pamba 259,431 sawa na asilimia 49.14 ya wakulima 527,938 kutoka Mikoa 11 inayolima pamba hapa nchini wanatumia nafasi mpya za upandaji wa zao hilo ambazo ni sm60 x sm 30. Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Tabora, Katavi, Singida, Morogoro, Dodoma Kigoma na Simiyu ambayo imefikiwa na mradi wa Cotton Victoria. Hili ni ongezeko la aslimia 6.14 ukilinganisha na misimu miwili iliyopita.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti cha TARI Ukiriguru Dkt Paul Saidia ambaye pia ni mwanasayansi kiongozi wa utafiti wa pamba nchini wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano mkuu wa kamati tendaji kitaifa ya mradi wa Cotton Victoria unaofadhiliwa na Serikali ya Brazil kupitia Shirika la Maendeleo la ABC.
“Wakulima wengi wanahamasika sana na hii teknolojia ya upandaji kwa nafasi mpya kutokana na tija kubwa inayopatikana. Sasa hivi kuna wakulima wanalenga kupata hadi Kg 3,000 kwa ekari tofauti na Kg 2,000 hadi Kg 2,500 wanazopata hivi sasa” Amesema Dkt Saidia katika Mkutano huo uliofanyika Aprili 10 2025 katika kituo cha Ukiriguru Mkoani Mwanza.
Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo cha pamba kutoka Wizara ya Kilimo, Mamlaka za serikali za Mikoa na Wilaya, taasisi za Serikali zikiwemo Bodi ya Pamba (TCB) na TOSCI.
Wakati akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Bi Johari Samizi amesema ni vema kuongeza hamasa ya kutangaza teknolojia ya upandaji wa pamba kwa nafasi mpya ili kuwafikia wakulima wengi nchini na hatimaye kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Bw. James Shimbe amepongeza utafiti unaofanyika TARI ambao kwa sehemu kubwa umechangia mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.
“Tumeshapata mbegu kutoka Pakistani kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa pamba, na utafiti wa mbegu hizo unaendelea ili kupata mbegu kinzani kwa magonjwa na ukame” Amesema Bw. Shimbe.
Naye Ndg Samson Poneja Afisa kutoka Wizara ya kilimo amesema mradi wa Cotton Victoria sasa unatoa matokeo tarajiwa ambayo yatasaidia kuimarisha tasnia ya zao la pamba nchini na kwamba Wizara kupitia TARI na TCB inaendelea kuimarisha soko la zao hili ili wakulima wanufaike zaidi na jitihada wanazofanya katika uzalishaji.
Social Plugin