Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile
Na Regina Ndumbaro- Songea .
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uchaguzi wa viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), utakaofanyika tarehe 5 mwezi huu katika ukumbi wa Bombambili, Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Hunt Club, Ruhuwiko, Manispaa ya Songea, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, akiwa na Makamu wake, Bakari Machumu, wameelezea lengo kuu la uchaguzi huo.
Wamesisitiza kuwa uchaguzi huu utahusisha nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na Kamati ya Uhariri Tanzania, huku wakiweka mkazo katika kudumisha umoja, upendo na haki katika mchakato huo.
Viongozi hao pia wameeleza kuwa wakati wa uchaguzi mara nyingi hutokea vitendo vya kuchafuana kwa kutumia mitandao ya kijamii, jambo ambalo wanapinga kwa nguvu zote.
Wamesisitiza kuwa kampeni za uchaguzi zinapaswa kuwa za kistaarabu na zenye kujenga mshikamano ndani ya tasnia ya habari.
Aidha, Mwenyekiti wa TEF amewashukuru viongozi wa mkoa wa Ruvuma, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, na Katibu Tawala kwa ushirikiano wao.
Pia amewapongeza wakurugenzi wa vyombo vya habari kwa kufanikisha maandalizi ya uchaguzi huu kwa kufadhili na kusimamia utoaji wa taarifa kwa umma.
Uchaguzi huu unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha tasnia ya habari nchini na kuhakikisha viongozi wapya wanaendelea kusimamia maadili na maslahi ya wahariri na wanahabari kwa ujumla.
Social Plugin