Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MLOLWA AHIMIZA MALEZI, UPANDAJI MITI NA KUCHAGUA VIONGOZI BORA


Na Sumai Salum-Kishapu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga Ndg. Mabala Mlolwa amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kishapu na maeneo ya Mkoa huo kupanda miti kwa wingi ili kukabiliana na mabadiliko tabia nchi.

Mlolwa ameyasema hayo leo Aprili 9,2025 alipokuwa kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya Jumuiya ya  Wazazi Kimkoa yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Bunambiyu Kata ya Bunambiyu Wilayani Kishapu Mkoani humo akiwa ndiye mgeni rasmi.

"Viongozi wa Jumuiya ya wazazi na wananchi wengine Leo kwenye mkutano wetu huu bila haya matent pengine tusingepata pa kukaa hivyo tuongeze kasi ya kupanda miti kwa wingi pamoja na mazuri mengi yanayofanywa na Jumuiya hii miti ni muhimu kwenye mazingira yetu",amesema Mlolwa

Pamoja na mambo mengine Mlolwa ameihimiza Jumuiya hiyo kusimamia maadili ya watoto,maadili kwenye Jumuiya zingine pamoja na Chama kwa ujumla ikiwa wao wamebeba hazina njema ya malezi bora kama Jumuiya mama.

Mlolwa amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi mazuri kwa kuboresha miundombinu ya sekta mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji,barabara,reli ya mwendokasi pamoja na usafiri wa anga.

Amewataka wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi ili kushika nafasi mbalimbali Halmashauri kuu kutenda  haki kwa  kupitisha wagombea wanaowasitahili wananchi na sio wanachama wa Chama hicho pekee.

Nae mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Shinyanga John Siagi amesema wanayofuraha kuadhimisha wiki ya wazazi kutokana na utekelezwaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM  kwa vitendo hasa suala la elimu bure ambapo wananchi wamejitoa kuwapeleka watoto shule.

"Kwa mantiki hiyo tunayo furaha kwani Rais Samia Suluhu amepanua demokrasia na Sisi tumekuwa sehemu ya maamuzi kuteua wagombea hivyo tutahakikisha tunatetea Chama chetu kupata ushindi wa kishindo hapo baadae kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu" amesema Siagi

Siagi ameongeza kuwa Jumuiya hiyo baada ya kugundua uwepo wa changamoto ya upungufu wa nyumba za watumishi ndani ya mkoa wa Shinyanga wameanza ujenzi huku wakikusudia ifikapo mwaka 2027 mkoa huo kutokuwa na changamoto hiyo ili watumishi watimize wajibu wao kwa weledi.

Aidha amewataka viongozi wa matawi na Kata kutembelea shule na kuzungumza na wanafunzi wabaini changamoto zinazowakabili kwa lengo la kupunguza ama kuondoa kabisa masuala ya ukatili katika Mkoa huo na kuwaelimisha pia.

Akisoma taarifa ya Jumuiya ya wazazi Katibu Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Shinyanga Regina Ndulu amesema Jumuiya hiyo ina miaka sabini sasa ambapo huadhimishwa kila mwaka April 6 ikiwa na  lengo la kusimamia sera za Chama Cha Mapinduzi ikijikita kwenye masuala ya  Elimu,malezi,afya na mazingira. 

Maadhimisho hayo yameambatana na upandaji miti pamoja  na ushuhudiaji ujenzi wa madalasa shule ya sekondari Bunambiyu 
Katika kipindi cha miaka mitano, shule hiyo ikipokea zaidi ya Tsh milioni 166 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi, na matundu ya vyoo,

Maadhimisho ya wiki ya  Jumuiya ya wazazi yameambatana na kauli mbiu isemayo Ushindi wa CCM  mwaka 2025 Jumuiya ya wazazi mstari wa mbele kazi na utu tunasonga mbele.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com