Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAYOMBO: VYOMBO VYA HABARI NI NGUZO KUU KATIKA UKUSANYAJI MAPATO


Mkurugenz wa elimu ya walipa kodi Richard Kayombo akiwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma Nicodem Mwakilembe akizungumza baada ya uchaguzi wa Wahariri Tanzania (TEF)Ukumbi wa Bombambili uliopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma. 

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, amesema kuwa vyombo vya habari ni nguzo kuu katika mafanikio ya ukusanyaji wa mapato nchini. 

Akizungumza katika Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika katika Ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea, Kayombo amesema ushirikiano uliopo kati ya TRA na wahariri wa vyombo vya habari umechangia kwa kiasi kikubwa kuvuka malengo ya mapato kwa miezi tisa mfululizo.

Akiwasilisha salamu za Kamishna Mkuu wa TRA katika mkutano huo wa uchaguzi wa viongozi wa TEF, Kayombo Amesema kuwa wanahabari wamekuwa daraja muhimu la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudai risiti na kulipa kodi. 

Amesisitiza kuwa bila mchango wa vyombo vya habari, jitihada za kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari zisingekuwa na mafanikio ya kiwango kilichofikiwa.

Kayombo ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, TRA imeweza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na wanahabari kwa niaba ya wananchi, jambo lililosaidia kuongeza imani ya walipa kodi kwa mamlaka hiyo. 

Amesema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yamekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya miundombinu, hasa sekta za usafiri wa barabara na anga.

Katika kuendeleza mafanikio hayo, Kayombo amewataka wahariri kuendeleza juhudi za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa ushirikiano na TRA, huku akiweka bayana kuwa elimu kwa mlipa kodi ni silaha muhimu katika kukuza mapato ya taifa. 

Ameahidi kuwa TRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na wahariri katika kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila Mtanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com