Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHERIA KANDAMIZI ZINAVYOKWAMISHA UHURU WA HABARI ZANZIBAR

 

Na Masanja Mabula

SHERIA ni mfumo wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza matendo yao na mahusiano yao pamoja na kutoa uhuru na haki kwa kundi au jamii husika.

Mifano ya kanuni hizo ni katika nchi, familia, ukoo, shule, ofisi,taasisi za serikali na binafsi.

Umuhimu mkubwa wa sheria kwa jamii ni kuwasaidia kuishi kwa amani na kujiletea maendeleo na ustawi katika nyanja mbalimbali kama kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi na hata kiroho.

Kwa tafsiri hiyo ina maanisha kwamba kila jamii au kundi linatakiwa kuwa na makubaliano ambayo yataweka sheria ambazo ni rafiki na zinazoendana na wakati na sio kukandamizi kundi au jamii husika.

Hivyo jamii yoyote haiwezi kuenenda au kukaa pamoja pasipo kuwa na sheria/kanuni za kuwaongoza.

Lakini sheria zikiwa zinakinzana na maendeleo na kundi au jamii husika zinapaswa kubadilishwa au kufutwa ili kusiweko na malalamiko ya baadhi ya jamii kunyimwa uhuru wake.

Ukakasi wa sheria unaweza kuzorotesha hata shughuli za maendeleo kwani wahusika watakuwa hawana uhuru wa kufanya kazi zao kwa ufanisi na weledi kwa sababu ya kukosa sheria rafiki ambazo zitawalinda wakati wa utekelezaji wa kazi zao.

Makala haya  inaenda kuangalia Sheria  Namba 5 ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Zanzibar ya mwaka 1988, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 1997, ambapo ndani yake vimo vifungu ambavyo bado vinaukakasi kwa wadau wa habari na wandishi wa habari.

Miongoni wa waandishi wa habari waliozungumza na Makala hii na kutoa maoni yao ni Salum Vuai ambaye ameshauri kifungu hicho kiondoshwe ili kutoa uhuru wa waandishi wa habari kuchapisha na kutangaza habari zao kwa ufanisi. 

Anasema kifungu cha 27 (1) kinampa Mamlaka Ofisa yeyote wa Polisi, kukamata gazeti lolote, popote litakapoonekana limechapwa au kuchapishwa au ambalo kwa maoni yake tu, atalituhumu kuchapishwa kinyume na sheria.

“ Kifungu hiki kwa maoni yangu kinapaswa kuondoshwa kabisa ndani ya sheria hii, kwani askari anaweza kuamka vibaya au kakerwa tu na mwandishi mmoja na yeye kutumia fursa hiyo kukamata gazeti; hapa uhuru wa habari uko wapi?” anahoji Salum Vuai.

Aidha ameshauri kutafutwa njia nyingine mbadala ikiwa ni pamoja na kutumia bodi au taasisi za kihabari likiwamo Baraza la Habari Tanzania-MCT-, Vilabu vya Waandishi wa Habari na wadau wengine wa habari (hawa watumiwe kufanya nini?).

“Chombo cha habari kinaandika na kutangaza ikiwa ni pamoja na kufichua baadhi ya maovu, jambo ambalo baadhi ya viongozi hawapendi hivyo afisa wa polisi anaweza kutumia fursa hiyo kwenda kukamata gazeti; hii haingii akilini katika ulimwengu huu wa utandawazi” alisisitiza.

Naye Shaaban Ali Abeid (huyu ni nani?) amefafanua kwamba hata kifungu cha 14 (1) kinachomlazimisha mchapishaji wa gazeti lililochapwa Zanzibar kwa kila siku na kwa gharama zake, kuwasilisha nakala mbili kwa Mrajisi wa magazeti.

Shaabani amefahamisha kuwa cha kusikitisha ni kwamba nakala hizo ziwe kwenye aina ya mfumo wa karatasi zile zile zilizochapishwa kwa ajili ya kusambazwa au kuuzwa.

“Kifungu hiki kimepitwa na wakati katika zama hizi ambazo gazeti unaweza kulipata mtandaoni, Kwani licha ya gharama anazopata mchapishaji wa gazeti, pia analazimishwa aingie gharama nyengine kupeleka nakala za gazeti kwa Mrajis hapa ni kuzidi kumuongezea gharama zisizo za msingi mchapishaji,” anasema.

Kwa upande wake Mwiaba Kombo Mtangazaji wa Redio Jamii Micheweni anasema  kifungu cha 27 (3) kinampa mamlaka hakimu kumuamuru afisa yeyote wa cheo cha mkaguzi au zaidi, ikiwa ana sababu ya maana ya kuamini kwamba, atachelewa kupata hati ya upekuzi anaweza kutekeleza uwezo alionao kwa mujibu wa sheria.

“Kifungu hiki siyo rafiki kwa uhuru wa habari nchini,” anasema. 

"Ikiwa Afisa wa Polisi atakuwa na ugomvi na mwandishi, anaweza kufanya upekuzi au kukamata gazeti, hali ambayo itasababisha taharuki katika vyombo vya habari,’’ anaongeza Mwiaba.

Mwanasheria Shoka Khamis Ame amesema ni vyema kifungu kingeainisha askari mwenye cheo cha juu na sio askari yeyote kupewa mamlaka makubwa namna hiyo. 

“Hapa sheria ni bora ingeainisha askari mwenye cheo cha juu kama RPC na sio askari yoyote kuamuriwa na Hakimu kufanya upekuzi wa gazeti”alishauri.

Aidha Shoka ameshauri kuwa Afisa  Polisi asipewe mamlaka hayo na badala yake iundwe bodi inayojumuisha wataalamu wa kada ya habari na wanasheria ili ifanye uchunguzi wa tuhuma zilizowasilishwa na ikithibitika chombo kimekiuka sheria ndipo kichukuliwe hatua.

Januari 24, 2023, akiwasilisha ripoti ya habari, iliyofanyiwa mapitio na TAMWA   Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Internews kuhusu sheria zinazokinzana  na uhuru wa habari, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dk. Mzuri Issa alisema vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kuchangia maendeleo ya nchi. (kwa hiyo?)

“Akitolea mfano mchango za sheria No 8 ( 27), (I) ya wakala wa Habari Magazeti Vitabu ambacho kinaeleza afisa yoyote wa Jeshi la Polisi anaweza anaweza kuzuia au kukamata gazeti lolote lile lisichapishwe iwapo atashuku linakwenda kinyume na  miktana ya kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza” Mwisho wa kunukuu.

Mkurugenzi wa Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake  TAMWA Zanzibar pichani akifafanua jambo kwenye mkutano wa wadau wa habari  Zanzibar mwengine ni Shifaa Said Hassan .

Hitimisho

Sheria ni msingi wa uhai wa jamii yoyote ile iwe kubwa au ndogo, zote zinahitaji uwepo wa sheria maana pasipo sheria kila mmoja atafanya atakayo kufanya na kutakosekana amani na uthabiti kwa maisha ya watu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com