Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog Songea
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Damas Ndumbaro, amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono wahariri na wanahabari nchini ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na katika mazingira bora.
Ametoa kauli hiyo leo katika Ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, alipokuwa akizungumza katika Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), unaolenga kujadili mustakabali wa tasnia ya habari nchini.
Waziri Ndumbaro amewataka wahariri na wanahabari kuwa na moyo wa kujituma, kushikamana, na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, huku akiahidi kuwa serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha taaluma ya habari inathaminiwa na kulindwa.
Aidha, ametumia fursa kuwaomba Watanzania wote kuendelea kuiunga mkono serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ya kazi kubwa na maendeleo makubwa yanayoendelea kushuhudiwa chini ya uongozi wake.
Akitumia nafasi hiyo kumkaribisha mgeni rasmi wa mkutano huo, Katibu wa CCM na mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Emanuel Nchimbi, Waziri Ndumbaro amempongeza kwa mchango wake mkubwa wakati alipokuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini.
Ameeleza kuwa Dkt. Nchimbi alijenga shule na ofisi ya CCM kwa kutumia rasilimali zake binafsi, jambo linaloonesha uwajibikaji na moyo wa kujitolea kwa ajili ya wananchi wa Songea.
Ndumbaro amesisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma wanaendelea kuwa na imani kubwa kwa Dkt. Nchimbi na kwamba wanaamini ataendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kuwaletea maendeleo kupitia serikali ya awamu ya sita.
Social Plugin