Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA MIFUGO WATAKIWA KUFUATA SHERIA KUHUSU HUDUMA ZA MIFUGO

Dkt. Caroline Uronu

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma.

Baraza la Veterinari Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi limewataka wadau wote wa mifugo nchini kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha utoaji holela wa huduma za mifugo.

Hayo yameelezwa na Dkt. Caroline Uronu kutoka ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Baraza la Veterinari Tanzania, alipokuwa akizungumza katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

Dkt. Uronu amesema kuwa wamefika Songea kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya baadhi ya wadau kutoa huduma za mifugo bila kuwa na uhalali wa kisheria.

Dkt. Uronu amefafanua kuwa si kila mtu anaruhusiwa kutoa huduma hizo, bali ni wale tu waliopata mafunzo rasmi na wenye taaluma husika.

Amesisitiza kuwa huduma za wanyama zina mipaka yake na zinapaswa kutolewa na wataalamu waliothibitishwa, ikiwa ni pamoja na madaktari wa wanyama na wasaidizi wao maarufu kwa lugha ya Kiingereza kama (veterinary paraprofessionals).

Hata hivyo, amebainisha kuwa hata wataalamu hawa wanapaswa kufuata mipaka ya taaluma zao bila kuzivuka kiholela.

Katika tukio hilo, Baraza la Veterinari lilimbaini Bwana Agano Albano kutoka Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kutoa huduma za matibabu ya mifugo bila kuwa na uhalali wa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha Sheria ya Veterinari Tanzania, mtu asiye mtaalamu wa mifugo haruhusiwi kutoa huduma hizo, na adhabu kwa kosa hilo ni kifungo cha mwaka mmoja au faini ya Shilingi milioni moja.

Dkt. Uronu ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika dhidi ya watu wanaojihusisha na huduma hizo bila sifa stahiki.

Kwa upande wake, Bwana Agano Albano aliyekumbwa na tukio hilo, amekiri kosa hilo na kusisitiza umuhimu wa watu kufuata sheria kwa kufanya kazi kulingana na taaluma walizosomea.

Ametoa mfano wa yeye mwenyewe, ambaye hajasomea afya ya wanyama lakini alijichukulia jukumu la kutoa matibabu ya mifugo kinyume cha sheria.

Ameahidi kuwa atatumia uzoefu wake kuwaelimisha wengine juu ya umuhimu wa kuheshimu taaluma.

Dkt. Seria Masole Shonyela kutoka Manispaa ya Songea amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Agano ni kinyume cha sheria na kinapaswa kukemewa.

Ameongeza kuwa halmashauri ya manispaa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna sahihi ya kupata huduma za mifugo na umuhimu wa kutumia wataalamu waliothibitishwa na Baraza la Veterinari Tanzania.
Dkt. Caroline Uronu Kutoka Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Baraza la Veterinari Tanzania
Dkt. Caroline Uronu akiwa pamoja na Dkt. Seria Masole Shonyela kutoka Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma pamoja Dkt. George Mtinda kutoka Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Baraza la Veterinari Tanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com