Na Lydia Lugakila _ Bukoba
Mkurungezi wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Jacob Nkwera amewahimiza Wananchi katika Manispaa ya Bukoba kuendeleza suala la usafi katika mji huo pamoja na maeneo ya makazi yao ikiwemo pia maeneo yao ya Biashara ili kujikinga na magonjwa mbali mbali ya kuambukiza yanayoweza kujitokeza hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazonyesha Mkoani humo.
Nkwera ametoa kauli hiyo Aprili 4,2025 alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake.
Amewahimiza Wananchi katika Manispaa hiyo kuhakikisha wanatunza mazingira yanayowazunguka ili yawe safi na salama kwa mujibu wa sheria ndogo ya mwaka 2018 inayomtaka kila mmoja katika eneo lake analoishi au anapofanyia Biashara kuwa safi kwa mita tano kushoto, kulia, mbele na nyuma.
"Kwenye majumba yetu pawe safi pia kuna makampuni ya uzoaji taka tulioingia nao mkataba yanafanya kazi kwenye mitaa hivyo niwaombe wananchi mtoe ushirikiano kwa kulipia kwani viwango vilivyowekwa ni vidogo",amesema kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa wao kama manispaa watahakikisha suala la usafi linazingatiwa ili wananchi wake waondokane na magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu.
Hata hivyo Nkwera ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazonyesha ikiwemo kudhibiti watoto kutochezea maji yaliyotuama, ikiwemo pia kudhibiti madimbwi ya maji ili kuepukana na magonjwa mbali mbali.
Social Plugin