
Na Regina Ndumbaro-Masasi.
Diwani wa Kata ya Migongo, Halmashauri ya Mji Masasi, Mheshimiwa Ismail Kalindima, amefariki dunia mnamo tarehe 11 Aprili 2025 katika Hospitali ya Mkomaindo, Masasi Mjini, mkoani Mtwara.
Mheshimiwa Kalindima, ambaye alizaliwa tarehe 1 Juni 1961, alikuwa diwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano.
Ameacha mjane, watoto watatu na wajukuu wanane.
Mazishi ya Mheshimiwa Kalindima yamefanyika katika kijiji cha Mbonde, nje kidogo ya mji wa Masasi, ambapo mamia ya waombolezaji wamehudhuria kumpa heshima za mwisho.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Bi Rachel Kassanda, ameshiriki katika mazishi hayo na kutumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wanamasasi kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, CPA Norbert Shee amekabidhi rambirambi ya Shilingi laki tatu kwa familia ya marehemu na kuwasilisha salamu za pole kutoka kwa mkuu wa mkoa.
Ameeleza jinsi ambavyo mkoa umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiongozi huyo aliyekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kata yake.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Masasi, Bi Mariam Kasembe, ametoa salamu za pole kwa familia na kueleza kuwa chama kimepoteza kiongozi mwenye mchango mkubwa, na kwamba kifo cha Mheshimiwa Kalindima ni pigo kwa Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, ameeleza kuwa CCM itaendelea kuwapa ushirikiano wanafamilia katika kipindi hiki kigumu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mheshimiwa Sugu, amezungumza kwa niaba ya baraza la madiwani na kueleza kuwa baraza hilo linaungana na familia ya marehemu katika maombolezo.
Amesema marehemu Kalindima alikuwa kiongozi shupavu na aliyetoa mchango mkubwa kwenye kamati ya mipango miji.
Amemtaja kama mtu aliyejitoa kwa dhati katika utumishi wa umma na maendeleo ya wananchi wa kata ya Migongo.
Social Plugin