
Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog
Wanachama 200 wa Chama cha ACT Wazalendo, akiwemo Katibu wa Chama hicho Jimbo la Tunduru Kusini, Saidi Mponda, pamoja na Diwani wa Kata ya Mchoteka, Sefu Hassan Dauda, wamejiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Uamuzi wao wa kuhama ACT Wazalendo na kujiunga na CCM umetokana na kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
viongozi hao waliotoka ACT Wazalendo wamesema wamevutiwa na namna Serikali ya CCM inavyojitahidi kuboresha sekta za miundombinu, afya, elimu na uchumi kwa ujumla.

Wameeleza kuwa maendeleo yanayoonekana katika wilaya ya Tunduru na maeneo mengine nchini ni kielelezo cha uongozi imara wa CCM, hivyo wakaona ni busara kujiunga na chama hicho ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo hayo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mlimgoti, wilayani Tunduru, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewapongeza wanachama hao kwa uamuzi wao wa kujiunga na CCM.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi ya maendeleo na akatoa wito kwa wanachama wa vyama vingine kujiunga na chama hicho ili kushirikiana katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.
Aidha, Dkt. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu dhamira ya CCM kuendelea kusimamia maendeleo na kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na rasilimali za nchi.
Amesema kuwa Serikali inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Watanzania wote kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote.
Amesisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na mshikamano na utulivu ili miradi ya maendeleo iweze kuwanufaisha wananchi wote.

Social Plugin