
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emanuel Nchimbi akizungumza wakati wa Mkutano maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog Songea
Dkt. Emanuel Nchimbi, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, amepongeza hatua ya kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akisema ni kielelezo cha dhamira thabiti ya kuimarisha taasisi hiyo kwa misingi ya demokrasia na uwajibikaji.
Akizungumza akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Maalum wa TEF uliofanyika leo katika Ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Dkt. Nchimbi amesema uchaguzi huo ni uthibitisho wa utayari wa wahariri kulinda uhalali wa kiuongozi kupitia njia halali na shirikishi.
Amesisitiza kuwa mahusiano bora kati ya viongozi na wanachama ndani ya taasisi yoyote hujenga msingi imara wa maendeleo, na kwamba juhudi za TEF kuendesha uchaguzi wa wazi ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini.
Aidha, Dkt. Nchimbi amewatakia heri waandishi wa habari Deodatus Balile na Bakari Machumu waliochukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, akieleza kuwa hatua yao inaonesha ujasiri na dhamira ya kulinda misingi ya uongozi bora.
Dkt. Nchimbi ameeleza kuwa jamii inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kujenga taifa kupitia utoaji wa habari sahihi kwa wananchi.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza wahariri na waandishi wa habari kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda amani ya nchi kupitia taaluma yao.
Amesema kupitia Ilani ya CCM, serikali inatambua mchango wa wanahabari na itaendelea kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kama sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.
“Tanzania imepiga hatua kwa asilimia 50 katika kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo hivi ni muhimili muhimu wa kudumisha amani,” ameeleza.
Ameahidi kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya habari nchini, ikiwemo kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari pamoja na kuboresha mazingira ya kiuchumi kwa vyombo vya habari.
Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuandika habari zinazojenga mshikamano wa kitaifa, badala ya zile zinazochochea chuki, na kuwatakia wahariri uchaguzi salama na wenye mafanikio.
Social Plugin