Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI NANE KUTOA HUDUMA BURE ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA ZAIDI YA 20



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Wiki ya Afya 2025 ikiwa inaendelea Jijini hapa, wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa zaidi ya 20, ikiwemo magonjwa ya afya ya akili.

Huduma hizo zinatolewa bure na wataalamu bingwa kutoka hospitali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Hospitali za Mirembe, Benjamini Mkapa, Bugando, Moi, KCMC, Ocean Roads na Kibong'oto.

Huduma hii imeanza rasmi tarehe 3 Aprili 2025 na inatarajiwa kumalizika tarehe 8 Aprili 2025, huku huduma mbalimbali za upimaji na uchunguzi wa awali zikiendelea kutolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 5,2025 katika Banda la Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Veronica Lymo amesema Wataalamu hao wanatoa huduma za bure kuhakikisha wananchi wanapata uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na kuweza kuyakabili.

"Lengo la wiki hii ni kutoa huduma za uchunguzi wa awali kwa watanzania wote, wananchi wanapaswa kujitokeza ili kugundua matatizo ya afya ya akili mapema na kuweza kupatiwa matibabu sahihi,

tunawakaribisha kwa wingi ili kuhakikisha tunawasaidia mapema. Ikiwa mtu atapata msaada mapema, tunaweza kuzuia madhara mapema., "amesema Dkt. Veronica.

Ameeleza kuwa wagonjwa wengi wanaoenda Hospitali ya Mirembe na kugundulika kuwa na matatizo ya Afya ya akili ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 40.

Ametaja changamoto zinazowakumba na kusababisha hali hiyo mara nyingi ni za kisaikolojia au kibailojia.

" Ili kuondokana na changamoto hizi, uchunguzi wa awali ni muhimu, na wananchi wanapaswa kufahamu kwamba magonjwa ya akili yanaweza kudhibitiwa ikiwa yatagundulika mapema.

Dkt. Lymo amebainisha kuwa hospitali hiyo inatoa elimu kuhusu afya ya akili na magonjwa ya akili, na wamefanikiwa kufikia mikoa mitano ili kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa afya ya akili.

Naye Dkt. Abasi Msaji kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili amesema kuwa hospitali yao inatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu, na huduma za uzito. Aliongeza kuwa hospitali hiyo pia inatoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine ya ndani.

Doris Mgaji mkazi wa Dodoma Makulu, ameelezea furaha yake kutokana na huduma zinazotolewa, akisema kuwa anapenda huduma hizi ziwe endelevu kwa sababu hospitalini huduma ni ghali na foleni ni ndefu. "Tunaomba kila Mtanzania aweze kufika Jakaya Kikwete ili kupata huduma nzuri na rafiki," alisema Masawe.

Wananchi wanaopima katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete wanapata huduma za upimaji wa magonjwa kama vile Saratani ya Matiti, Saratani ya Mlango wa Kizazi, Kisukari, Shinikizo la Damu, Kifua Kikuu, pamoja na huduma za kinywa na meno, macho, na uzazi wa mpango. Pia, kuna huduma za chanjo ya HPV (Saratani ya Mlango wa Kizazi) na msaada wa kisaikolojia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com