Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jumla ya Shilingi bilioni 129.7 zimetumika kugharamia ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, ambalo linatajwa kuwa ni moja ya miradi mikubwa zaidi ya kimkakati kuwahi kutokea nchini. Jengo hili pia linatarajiwa kuwa kubwa zaidi barani Afrika na kushika nafasi ya sita kwa ukubwa duniani.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, alieleza hayo leo, Aprili 3, 2025, katika mkutano wake na vyombo vya habari, ambapo alisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atazindua rasmi jengo hilo Aprili 5, mwaka huu.
Jengo hilo linajumuisha sehemu tatu kuu: Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani, na Mahakama Kuu. Ujenzi wake umefadhiliwa kwa fedha za ndani, ikiwemo kodi za wananchi, na linatarajiwa kuwa na ukubwa wa mita za mraba 63,244. Aidha, jengo hili limejengwa kwa kuzingatia ubora wa kipekee na lengo la kudumu kwa zaidi ya miaka 100.
Prof. Gabriel amefafanua kuwa jengo hili litakuwa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA, akili bandia, na roboti zitakazosaidia wananchi katika kutafuta ofisi mbalimbali, pamoja na sehemu ya kutua helikopta. Jengo hili linatarajiwa kuwa kitovu cha utoaji haki nchini, na limejengwa kwa lengo la kuboresha huduma za mahakama na kuongeza ufanisi wa kazi za utawala.
Mbali na uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama, Rais Samia pia atazindua miradi mingine miwili, ikiwemo jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama lenye ghorofa sita, lililogharimu Shilingi bilioni 14.3, pamoja na makazi ya majaji yenye thamani ya Shilingi bilioni 42.3.
Hafla hiyo ya kihistoria inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wageni 2,500, wakiwemo viongozi kutoka sekta mbalimbali za serikali, bunge, mahakama, mashirika ya kiraia, na viongozi wa dini.
Social Plugin