Na Woinde Shizza - Arusha
Katika jitihada za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usalama Mtandao nchini, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesisitiza umuhimu wa kujenga uchumi wa kidijitali wenye msingi wa usalama wa taarifa.
Akifunga mkutano wa nne wa jukwaa la wataalam wa usalama mtandao jijini Arusha, Dkt. Mwasaga amesema wanatengeneza mnyororo wa ubunifu unaojumuisha wanafunzi, watafiti na wadau wa teknolojia ili kuimarisha usalama wa mitandao.
Ameeleza kuwa matumizi ya kidijitali yamejikita kwenye nguzo tano ambazo ni ujuzi wa kidijitali, usalama na imani kwa watumiaji, mawasiliano ya kidijitali, uchumi wa kidijitali, na ubunifu Vilevile, amebainisha kuwa wanaendelea kuunda programu zitakazosaidia kukuza uelewa wa usalama mtandao, hasa kwa wanafunzi kutoka vyuo kama UDOM na Chuo cha Uhasibu Arusha.
Dkt. Mwasaga amesema mafanikio ya teknolojia pia yameongeza matukio ya uhalifu mtandaoni, hivyo kunahitajika ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo serikali, taasisi binafsi na watumiaji wa kawaida wa mtandao ili kulinda taarifa binafsi dhidi ya hatari zinazojitokeza.
Katika mkutano huo, wanafunzi wa UDOM walipata nafasi ya kuonyesha ubunifu wao kwa kuwasilisha programu ya ‘Sitapeliki’, inayolenga kukomesha utapeli wa mtandaoni , Linda Kasubi, mmoja wa wanafunzi hao, alisema wameshirikiana na TCRA kuhakikisha ujumbe huo unawafikia wananchi wengi.
Kwa upande wake, mwanafunzi Ibrahim Francis amesema jukwaa hilo limewasaidia kuelewa namna ya kushiriki kikamilifu katika mjadala wa masuala ya usalama mtandaoni na kuwaelimisha wenzao kuhusu tishio hilo linaloongezeka kila siku.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia huku ikihimiza kila Mtanzania kuwa na uelewa wa kutosha ili kujilinda dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.
Social Plugin