
Na Lydia Lugakila - Bukoba
Hayo yameelezwa na mwanasiasa ambaye pia ni mbobezi katika masuala ya uchumi na kilimo kutoka Mkoani Kagera Evance Kamenge wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Kagera waliotaka kufahamu mambo mbalimbali katika nyanja ya kiuchumi, Biashara na siasa kutoka kwake.
Kamenge amesema kuwa anaumia sana kila anapoanza kuzungumzia kilimo kwa sababu yeye anafanya kilimo kama chaguo sahihi japo vijana wengi wanakimbia kilimo na kubaki mjini wakizunguka na bahasha kutafuta kazi.
Amesema kuwa mkoa wa Kagera una bahati ya kuwa ardhi nzuri yenye rutuba lakini vijana wengi au baadhi ya watu hawajishughulishi na kilimo kwa aina yake hasa kilimo cha kahawa ambapo kilimo kimewekwa nyuma na kuonekana sio kazi rasmi.
Amesema vijana wengi wamekimbia kilimo kufanya kazi ya kuendesha pikipiki maarufu Boda Boda.
"Sisemi boda boda sio kazi hapana ni kazi tena nzuri ila vijana wengi wamekimbia uti mgongo wa uchumi wa Taifa lao kijana anaacha heka mbili hazijalimwa anakimbilia kuendesha pikipiki kwa miaka 20 na baada ya hapo maumivu ya mgongo yanakuwa tayari ambapo anakuwa hawezi kuendesha pikipiki tena lakini kama angepanda mibuni 100 na kuzalisha Kahawa kilo mbili ndani ya miaka 3 kijana angekuwa mbali kiuchumi "amesema Kamenge.
Ameongeza kuwa tatizo linakuja katika upande wa kukata tamaa kwa baadhi ya vijana na kutaka matokeo ya haraka.
Akizungumzia suala la uchumi amesema kuna kitu kiitwacho uchumi wa kifamilia ambao huo ndio uchumi mama ulioyakomboa mataifa 20 makubwa yenye nguvu duniani hivyo ni vyema vijana wakatambua kuwa uchumi wa kifamilia ndio njia pekee ya kuwapa utajiri na ajira wanayosumbuka nayo kila kukicha.
"Huwa napata taabu Sana mimi Kamenge ninaposikia watu wanalilia ajira pia napata taabu sana ninaposikia watu wanasema kilimo sio kazi niwaombe vijana watambue kuwa kilimo ndio Uti wa mgongo wa Nchi hii"amesema Mwana uchumi huyo.
Ameeleza kuwa, hata waasisi wa Taifa hili walitambua kuwa nchi hii ni ya Wakulima na.wafanyakazi na kuwa ni wakati sasa vijana kujikita katika kilimo na ufugaji ili kujikwamua kiuchumi.
Amewashauri wananchi Wilayani Misenyi kupambana na kuendeleza kilimo kwa faida kizazi cha sasa na cha baadae.
Social Plugin