Viongozi mbalimbali wa dini wa Kilutheri wakiwemo na waumini wakati wa hafla ya uzinduzi wa idara ya wanaume usharika wa Msamala Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro-Songea-Ruvuma
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ruvuma, Usharika wa Msamala, limeadhimisha Siku ya Wanaume kwa mafanikio makubwa, sambamba na uzinduzi rasmi wa Idara ya Wanaume ndani ya usharika huo.
Hatua hii inalenga kuwaunganisha wanaume, kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiroho na kijamii, pamoja na kuchochea maendeleo ya kanisa.
Uzinduzi huu ni hatua muhimu kwa kuwa unaleta jukwaa rasmi kwa wanaume kujadiliana, kushirikiana na kushiriki katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya kiroho na kijamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Jimbo la Songea, Hezironi Mhabuka, amesema maadhimisho haya yamefanyika ili kuhakikisha wanaume wanatambua nafasi na wajibu wao katika familia, kanisa, na jamii kwa ujumla.
Ameeleza kuwa majimbo mengine, kama Njombe, tayari yameanzisha idara hii hadi katika ngazi za familia, na sasa Dayosisi ya Ruvuma inafuata nyayo hizo kwa kuhakikisha wanaume wanajihusisha zaidi na masuala ya kanisa.
Mhabuka amesisitiza kuwa mpango huu utasaidia kujenga kanisa lenye mshikamano, ambapo kila mtu anajua wajibu wake.
Uanzishwaji wa Idara ya Wanaume katika Usharika wa Msamala, ambao ni makao makuu ya jimbo, ni hatua muhimu kwa kuwa usharika huo ndio wa kwanza kuanzisha idara hiyo ndani ya Dayosisi ya Ruvuma.
Lengo kubwa la idara hii ni kuhakikisha kuwa mpango huu unafikia dayosisi nzima ili wanaume waweze kushiriki mijadala ya kiroho, kushirikiana kutatua changamoto zao, na kuimarisha mshikamano wa waumini.
Pia, inatarajiwa kuwa idara hii itasaidia kuwajengea wanaume utayari wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kanisa na jamii kwa ujumla.
Waumini wa KKKT katika Usharika wa Msamala wameonyesha furaha yao kwa hatua hii, wakiamini kuwa itachangia kubadili mtazamo wa wanaume kuhusu majukumu yao.
Filippo Shantembo, mmoja wa waumini, amesema kuwa mafanikio yanayotarajiwa ni kuwafanya vijana wanaokua sasa kuelewa mapema nafasi na wajibu wao katika jamii.
Ameongeza kuwa kila mwanaume anapaswa kutambua umuhimu wake katika kanisa na familia, ili kujenga kizazi chenye maadili na mshikamano thabiti.
Kwa mafanikio haya, KKKT Dayosisi ya Ruvuma inaendelea kuhimiza ushiriki wa wanaume katika maendeleo ya kiroho na kijamii, ikiwa na matumaini kuwa idara hii itasaidia kukuza uwajibikaji miongoni mwao.
Hii ni hatua muhimu kwa kanisa, kwani inawapa wanaume nafasi ya kuimarisha uhusiano wao na Mungu, familia zao, na jamii kwa ujumla.
Social Plugin