Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE AKAA NA UJAUZITO KWA MIAKA MINNE SHINYANGA



Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Katika hali isiyo ya kawaida, mwanamke mmoja mkazi wa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga amebainika kuishi na ujauzito kwa zaidi ya miaka minne kabla ya kufanyiwa upasuaji ambao umebaini kuwa kiumbe aliyekuwa tumboni alikuwa tayari amefariki dunia.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 55, alipata ujauzito huo akiwa na miaka 51 na alishindwa kufahamu hali hiyo kwa muda mrefu, jambo lililompelekea kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji akiamini ni matatizo ya kawaida.

 Kwa mujibu wa maelezo yake, alikumbwa na hofu na aibu ya kijamii kutokana na mila na desturi potofu, hali iliyomfanya kukaa kimya kwa muda wote huo.

Baada ya hali yake kuwa mbaya, alifikishwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama na baadaye kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambapo amefanyiwa upasuaji.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Augustino Maufi, amesema baada ya vipimo, ilibainika kuwa alikuwa na mimba iliyotunga nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy) hali ambayo kitaalamu ni hatari na huweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya mama.

Dkt. Maufi ameongeza kuwa hali hiyo husababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo maambukizi kwenye mfumo wa uzazi na kwamba iwapo mama huyo angefika hospitalini mapema, hali hiyo ingaliweza kuzuilika.

Aidha, daktari huyo ametoa wito kwa wanawake wote walioko katika kipindi cha ujauzito kuhakikisha wanapata huduma katika vituo vya afya pindi wanapokumbwa na changamoto yoyote badala ya kutegemea tiba za jadi ambazo mara nyingi huchelewesha au kuzorotesha afya zao.

TAZAMA VIDEO HAPA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com