Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAWAKILI WATAKIWA KUJIVUNIA TAALUMA YAO



Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kimekutana Jijini Dodoma kufanya Mkutano wake Mkuu  ikiwa ni mwaka wa tatu tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Mkutano huo unatajwa kuwa ni fursa muhimu kwa mawakili hao wa serikali kwa kuwa pamoja na Mambo mengine utatumika  kujadili namna ya kukijenga chama kuwa chenye nguvu na ushawishi. 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Hamza Johari, ametumia mkutano huo kuwataka mawakili hao  kujivunia taaluma yao huku wakihakikisha wanachagua viongozi wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza na kutekeleza malengo ya Chama cha Mawakili wa Serikali.

Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho unaofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Mhe. Johari alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa mawakili wote wa serikali kujadili mustakabali wa chama chao pamoja na maendeleo ya sekta ya sheria kwa ujumla.
Mhe. Johari alibainisha kuwa lengo kuu la mkutano ni kutoa nafasi kwa wanachama kujadili changamoto, mafanikio na mikakati ya kuimarisha utendaji wao kwa kuzingatia ukuaji wa taaluma na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa viongozi wenye fikra pana na dira ya maendeleo, watakaoshirikiana na uongozi wa juu wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya chama.

Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Utawala wa Kisheria katika Utekelezaji wa Majukumu ya Serikali ni Nguzo Muhimu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”, Mhe. Johari amesema inatoa mwelekeo sahihi wa jinsi sekta ya sheria inavyopaswa kujipanga kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, aliwahimiza mawakili wa serikali kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi bila woga, na kuzingatia maelekezo kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com