Soko la Samaki Somanga Kilwa Mkoani Lindi
Wafanyabiashara wa Samaki wakiendelea na biashara za Samaki katika Soko la Samaki Somanga Kilwa Mkoani Lindi
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Samaki Soko la Somanga Kilwa Mkoani Lindi
**
Na Regina Ndumbaro-Lindi
Soko la samaki lililopo katika Kata ya Somanga, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi limekuwa chachu ya maendeleo kwa kuongeza fursa za ajira kwa vijana, wanawake na wananchi kwa ujumla.
Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya ukaguzi wa soko hilo iliyofanywa na diwani wa kata hiyo, maafisa wa serikali pamoja na wadau binafsi wa maendeleo, ambapo wameshuhudia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Somanga, Mheshimiwa Saidi Manjonjo amesema kuwa soko hilo limeleta ajira kwa watu wengi, hasa kina mama, katika nafasi mbalimbali kama usafi wa mazingira, ulinzi, uendeshaji wa biashara na shughuli nyingine nyingi.
Ameongeza kuwa soko hilo limeleta unafuu mkubwa kwa wananchi kwa kuwa limehamishiwa eneo lenye miundombinu bora, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Kata ya Somanga, Bi. Agness Paschal ameeleza kuwa soko hilo limefungua fursa nyingi mpya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa fremu za maduka, biashara ya kukaanga samaki, na uuzaji wa vyakula mbalimbali.
Amebainisha kuwa jitihada hizi zimewawezesha wakazi wa eneo hilo kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.
Wadau waliohudhuria ziara hiyo wametoa pongezi kwa juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuboresha huduma zaidi sokoni hapo.
Wamehimiza vijana na wananchi kutumia kikamilifu fursa zilizopo kwa manufaa yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Social Plugin