Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAFALI YA KWANZA KIDATO CHA SITA SHULE YA WASICHANA DKT. SAMIA YAFANYIKA NAMTUMBO




Baadhi ya Wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan wakiwa kwenye maandamano wakati wa mahafali ya kwanza shuleni hapo
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Wlaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dafrosa Chilumba,akizunguza na Wanafunzi,Walimu,Wazazi na Wageni waliofika kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha Sita ambapo jumla ya Wanafunzi 204 wanatarajia kuhitimu masomo yao.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Damas Suta,akiangalia maonyesho ya Kisayansi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wakati wa Mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya Shule hiyo.


Na Regina Ndumbaro _ Namtumbo. 


Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imefanya mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi 204 wanatarajia kuhitimu masomo yao mwaka 2025. 

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt Damas Suta, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amewapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na ustahimilivu waliouonyesha katika safari yao ya elimu. 

Dkt. Suta amewahimiza wahitimu hao kutambua kuwa mahafali ni hatua tu katika safari ndefu ya elimu na maendeleo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea na elimu ya juu au kuanzisha shughuli za kujitegemea huku wakitumia mitandao ya kijamii kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa.

Aidha, Dkt Suta amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shule na kufuatilia mienendo yao ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri maadili ya watoto hao. 

Amewasisitiza wanafunzi waliobaki shuleni kutokata tamaa bali wazidi kujituma katika masomo yao ili kuwa na maisha ya kitaaluma yenye mafanikio. 

Vilevile, amewapongeza walimu kwa kazi kubwa na ya kipekee waliyoifanya katika kufanikisha mafanikio ya wanafunzi hao, huku akiwasihi wazazi kuendeleza ushirikiano katika kuwahudumia watoto wao kitaaluma.

Kwa upande wa Mkuu wa Shule hiyo, Dafrosa Chilumba, amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2022 na kukamilika 2023 chini ya mradi wa SEQUIP unaolenga kuimarisha elimu ya sekondari kwa wasichana. 

Amesema shule hiyo jumuishi ina jumla ya wanafunzi 676 kuanzia kidato cha kwanza hadi sita, na ilianza kudahili wanafunzi wa kidato cha tano mwezi Agosti 2023. 

Hadi sasa, wanafunzi 204 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2025 katika tahasusi mbalimbali kama PCB, CBG, HGL, HGK, na HKL. 

Chilumba ameishukuru Serikali kwa kutoa Shilingi bilioni 4.450 kwa ujenzi wa shule hiyo ya kisasa lakini pia ameeleza changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo uhaba wa vifaa vya TEHAMA, viwanja vya michezo, vitabu, uzio wa shule, na upungufu wa walimu.

Awali katika risala ya wanafunzi iliyosomwa na Stella Magaho, wanafunzi wameelezea safari yao ya elimu tangu mwaka 2023 wakiwa wanafunzi wa kwanza wa kidato cha tano, na kueleza mafanikio waliyoyapata kitaaluma na kimidahalo hasa katika kukuza lugha ya Kiingereza. 

Mahafali hayo yamepambwa na maandamano ya wahitimu pamoja na maonyesho ya kisayansi yaliyokaguliwa na Dkt. Damas Suta, akiongozana na Mkuu wa shule Dafrosa Chilumba, kabla ya kuanza rasmi kwa hafla ya mahafali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com