Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Ridhiwani Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi duniani itakayofanyika Mkoani Singida Aprili 28 mwaka huu.
Hayo yameelezwa Aprili 23,2025 Jijini hapa na Waziri huyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na uwekaji wa mazingira salama mahali pa kazi.
Waziri Kikwete amesema siku hiyo pamoja na mambo mengine itaadhimishwa kwa kauli mbiu ya "nafasi ya akili mnemba na Teknolojia za kidigitali katika mapinduzi ya usalama na afya kazini"ikiwa imelenga kuhamasisha na kuwakumbusha waajiri kujiandaa kutumia akili mnemba katika uzalishaji na utoaji bora wa huduma.
" Teknolojia hii inaenda kuleta mabadiliko chanya ikiwemo machine na mifumo inayotumia akili mnemba kufanya kazi haraka,kwa usahihi bila kuchoka,ni vyema pia kutambua kuwa matumizi hayo hayamaanishi kupoteza ajira bali kuleta mabadiliko katika ajira, "amefafanua
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza mahitaji ya wataalam, mafundi wa mitambo ya kisasa na wasimamizi wa taarifa na mifumo ya akili mnemba.
Akizungumzia namna maadhimisho hayo yatakavyofana amesema, yataambatana na maonesho ya usalama na afya mahala pa kazi na wadau wengine ili kutoa elimu kwa umma na kubadilishana uzoefu miongoni mwao juu ya masuala ya usalama.
"Maonesho haya yatafanyika viwanja vya Mandewa -Singida ambapo pia Kutakuwa na kliniki ya uchunguzi wa afya za wafanyakazi kwenye magonjwa ya wanawake, afya ya akili, sukari, saratani na macho, " amesema
Social Plugin