Meneja wa TAMCU Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Marcelino Mrope akizungumza na Waandishi wa habari
Wakulima na wanachama wa TAMCU wakiwa kwenye mkutano
Na Regina Ndumbaro-Tunduru.
Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanda za Juu Kusini Tandahimba (TAMCU) kimepanga kujenga kiwanda kikubwa cha kubangua korosho katika Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Meneja wa TAMCU, Marcelino Mrope, wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa 22 uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Mrope amesema kuwa kiwanda hicho ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza thamani ya zao la korosho na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Mrope, kiwanda hicho kitaweza kubangua tani 3,500 za korosho kwa mwaka na kinatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni nne.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo mkubwa utaongeza mnyororo wa thamani wa korosho na kupunguza utegemezi wa kuuza korosho ghafi nje ya nchi, jambo ambalo litaongeza mapato ya ndani kwa wananchi na halmashauri.
Mrope ameziomba taasisi za kifedha kama CRDB Bank, benki ya ushirika inayotarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na taasisi nyingine za kifedha kuunga mkono juhudi hizo.
Amesema ushirikiano na wadau hao ni muhimu katika kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho na kuchochea maendeleo ya wakulima kupitia upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha.
Kuhusu faida za kiwanda hicho, Mrope amebainisha kuwa zaidi ya ajira 200 zinatarajiwa kutolewa kwa wakazi wa Tunduru, hatua itakayopunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.
Vilevile, uwepo wa kiwanda hicho utasaidia kuongeza bei ya korosho kwa wakulima, kuongeza mapato ya serikali kwa njia ya kodi, pamoja na kuimarisha uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa baadhi ya wakulima wa korosho wilayani Tunduru, akiwemo Bi Sharifa Mkwanda na Bw. Lesi Mesi, wameeleza kufurahishwa kwao na ujenzi wa kiwanda hicho.
Wamesema kuwa kiwanda hicho kitaleta matumaini makubwa kwao, hasa kwa kuongeza thamani ya mazao yao na kuwapatia bei nzuri ya korosho.
Social Plugin