Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JOWUTA YATAKA WAANDISHI WA HABARI KUTENDA HAKI KWA VYAMA VYOTE UCHAGUZI MKUU


Na Mwandishi wetu,Morogoro

Chama cha Wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini(JOWUTA),kimewataka waandishi wa habari nchini kuandika na kutangaza habari za vyama vyote kwa usawa huku,kikivitaka vyama vya siasa kutoingilia uhuru wa vyombo vya habari.

Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa,Mussa Juma ametoa wito huo katika ufunguzi wa mafunzo ya waandishi wa habari Kanda ya Mashariki na Pwani yaliyofanyika mkoani Morogoro April 24,2025.

Mafunzo hayo yanayoratibiwa na JOWUTA yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ),Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu nchini(THRDC) ,Taasisi ya wanahabari ya usaidizi wa jamii za pembezoni(MAIPAC) na Shirikisho la waandishi barani Afrika(FAJ).

Juma amesema, kuelekea uchaguzi mkuu,.wanahabari nchini wanapaswa kutenda haki kwa vyama vyote vya siasa.

"Tunataka katika uchaguzi mkuu ujao wanahabari tuzingatie sana maadili,tuache ushabiki wa vyama na wale wenye mapenzi na vyama bora wajiweke kando katika tasnia hadi uchaguzi upite",amesema.

Hata hivyo Juma, alivitaka viongozi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kuingilia uhuru wa wanahabari katika chaguzi.

Akitoa mada juu ya ulinzi na usalama kwa waandishi wakati wa uchaguzi,Juma amewataka wanahabari kujali usalama wao na usalama wa vyombo vyap vya kazi wakati wa uchaguzi na kabla.

"Kabla hujaandika habari fanya tathmini ya habari yako,inawagusa kina nani,je ina athari gani na kama inavitisho chukuwa tahadhari",amesema.

Afisa Uchaguzi wa Manispaa ya Morogoro,Shabani Duru akifungua mafunzo hayo amewataka waandishi wa habari kufanyakazi kwa weledi kuelimisha umma masuala ya uchaguzi.

Duru amesema, wanahabari ni wadau muhimu katika.uchaguzi mkuu na wataendelea kushirikisha katika mchakato wote wa uchaguzi.

Mwakilishi wa Mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu(THRDC),Wakili.Jons Sendodo  akitoa mada juu ya sheria za uchaguzi na kuripoti habari za uchaguzi amewataka wanahabari kuzijua sheria lakini kuzingatia ukweli,usahihi na masuala ya jinsia.

Wakili Sendodo, amewataka wanahabari  kutambua umuhimu wa usalama.wao kazini na kujua kuna vyombo vya kuwatetea wanapokabiliwa na majanga.

Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga akitoa mada juu ya maadili ya uandishi kuelekea uchaguzi mkuu,amesema maadili ya waandishi ni muhimu kuzingatiwa.

Amesema kuelekea uchaguzi ni vizuri waandishi kuandika ukweli,kujiepusha na habari za uzushi na upendeleo na upotoshaji.

Mafunzo hayo ya wanahabari yanaendelea katika mikoa ya Mbeya,Iringa na Njombe na baadae Arusha kwa waandishi wa Kanda ya Kaskazini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com