Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHAMA CHA WALIMU PWANI CHAPATA VIONGOZI WAKE


Mwalimu Alfred Peter Ringi akikabidhi kitabu chake cha historia ya mkoa wa Singida  kwa Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Bi. Susan Shesha
Mwalimu Alfred Peter Ringi akigawa zawadi ya vitabu vya Kiingereza alivyotunga yeye mwenyewe kwa baadhi ya walimu ambao pia ni wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT Taifa
Afisa kazi wa mkoa wa Pwani Bw. Metta Nahonyo akikabidhi cheti cha ushindi kwa mwenyekiti mteule wa CWT Mkoa wa Pwani Mwalimu Hamdani Kisoma
Mwenyekiti mteule wa CWT Mkoa wa Pwani Bw. Hamdani Kisoma
Viongozi waliopita bila kupingwa
Mjumbe wa Kamati ya utendaji Taifa kutoka mkoa wa Pwani Bw. Hubert Ngimi
Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Bi. Susan Shesha
KATIBU Tawala wa msaidizi Uchumi na Uzalishaji  wa mkoa wa Pwani , Shangwe Twamala akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT Mkoa wa Pwani


NA. ELISANTE KINDULU, KIBAHA

CHAMA cha walimu(CWT) mkoa wa Pwani kimepata viongozi wake kwa kipindi kingine cha mwaka 2025-2030.

Uchaguzi huo ulifanyika katika bwalo la polisi mjini hapa Aprili 23,2025 baada muhula wa uongozi wa Chama hicho kumalizika.

Nafasi zilizogombaniwa na idadi ya kura kwenye mabano ni nafasi ya Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Pwani, ambapo matokeo yalikuwa kama ifuatavyo;  Mwalimu Alfred Peter Ringi (17), Mwalimu Christian Sekione( 0 ), Mwalim Hamdani Kisoma(50),  Dkt. Joseph Awino (35) na Mwalimu Monica Vitalis (0). Hivyo mshindi alikuwa Mwalimu Hamdani Kasoma kutoka Wilaya ya Kibiti.

Kwa upande nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa wilaya za mkoa wa Pwani ilichukuliwa na Mwalimu Abdul Hamisi aliyepata kura (56) ambaye ni Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Mafia  dhidi ya Mwalimu Hamisi Kimeza aliyepata kura (46), ambaye ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Bagamoyo.

Nafasi walizoshinda wagombea bila kupingwa ni pamoja na  mweka hazina, mwalimu Abel Shiliye(Kisarawe), mwakilishi wa walimu vijana, Mwalimu Sultan Dihenga(Mafia), Mwakilishi wa walimu  wanawake , Mariamu Mpunga (Kisarawe), Mjumbe wa kamati ya utendaji Taifa Mwalimu Hubert Ngimi(Mkuranga), Mwakilishi wa walimu walemavu, Meshaki Lusumo (Kibaha).

Wagombea wengine walioshinda bila kupingwa ni Susan Shesha -mjumbe wa baraza kuu la Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA)Kibaha), huku nafasi za wajumbe wa mkutano mkuu wa TUCTA zilienda kwa Mwalimu Leila Kipole(Kibiti) na Abdul Dihunzi( Rufiji).

Kwa upande wa Kitengo cha walimu wanawake,wapiga kura walikuwa 34. Nafasi ya Mwenyekiti wa kitengo hicho iligombaniwa na walimu watatu. Aliyeshinda ni Mwalimu Sharifa Mngwali (24) kutoka Mafia dhidi ya wapinzani wake wawili waliopata kura 10 na mwingine 0 . Mweka hazina wa kitengo hicho iligombaniwa na walimu wawili ambapo Mwanaidi Kombo(Mkuranga) alishinda kwa tofauti ya kura moja dhidi ya mshindani wake wa karibu Jamila Omari kutoka Kibaha.

Nafasi ya Wajumbe wa walimu wanawake iligombaniwa na wagombea 6. Walioshinda ni Bahati Wendelini (11) kutoka Rufiji, Florence Ambonisye(8) kutoka Kibaha na Nyanjige Bukoma(7) kutoka  Bagamoyo, Huku nafasi ya walimu wanawake ikichukuliwa na Mwalimu Mariamu Mpunga (Kisarawe).

Mwenyekiti mteule wa CWT Mkoa aliwashukuru wajumbe kwa kumpigia kura za kutosha na kuahidi kuwatumikia walimu zaidi kuliko kukaa ofisini, huku akiahidi kushirikiana na viongozi wenzake pamoja na kuomba ushauri hata kwa washindani wake katika nafasi hiyo ili kukipeleka chama Mbele.

Akikaribishwa kuongea na wajumbe kwa niaba ya wagombea ambao kura zao hazikutosha, Mwalimu Alfred Peter Ringi aliwataka wajumbe kuvuja makundi na kuwa kitu kimoja huku akitoa zawadi ya vitabu vya kiingereza alivyotunga yeye mwenyewe kwa baadhi ya wajumbe wanaofundisha somo hilo katika shule za msingi na kitabu kingine cha Historia ya mkoa wa Singida kwa katibu wa CWT mkoa wa Pwani ikiwa ishara ya mkoa kutambua uwepo wa hazina ya walimu wenye ujuzi mbalimbali.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Afisa kazi wa Mkoa wa Pwani Bw. Metta Nahonyo kwa kuwaasa viongozi wateule kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wafanyakazi wanapunguza au kuondoa manung'uniko na migogoro mahala pa kazi.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Bi. Susan Shesha  aliisifu serikali kwa kusikiliza kero za walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja japo bado Kuna changamoto mbalimbali ikiwemo suala la kikokotoo.

Akifungua mkutano huo, Mgeni rasmi katika mkutano huo ,Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Pwani, Bw. Shangwe Twamala aliiomba CWT iweke mikakati kwenye shule ili kurudisha maadili ya watoto ambayo kwa sasa yameporomoka kwa kiasi kikubwa.

"Mtunze maadili ya ualimu kwa watoto na jamii, kwa kuwa jamii inawategemea kama kioo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kufundisha na kulea wanafunzi", alisema mgeni rasmi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 102 kutoka Wilaya zote za mkoa wa Pwani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com